Jaji Mkuu Martha Koome, amekashifu mashambulizi ya miundomsingi ya mahakama wakati wa maandamano ya Gen Z Juni 25,2025.
Kupitia kwenye taarifa, Jaji huyo Mkuu alisema kuwa uharibifu wa miundomsingi ya Mahakama, uhahujumu mfumo wa sheria na upatikanaji wa haki.
Kwenye taarifa hiyo iliyotolewa baada ya kuzuru Mahakama ya Kikuyu ambayo ni miongoni mwa miundomsingi ya serikali iliyoharibiwa na waandamanaji, Koome alidokeza kuwa licha ya katiba kutoa uhuru wa haki ya kuandamana kwa amani, imebainika kwamba wahalifu waliyaingilia maandamano hayo.
“Sehemu ya 37 ya katiba, inaruhusu mikusanyiko, kujieleza na maandamano. Hata hivyo, maandamanao hayo lazima yatekelezwe kwa kufuata sheria na bila kutumia silaha yoyote,” alisema Jaji Mkuu.
Alidokeza kuwa mashambulizi dhidi ya Mahakama yamedidimiza uwezo wa mahakama wa kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wakenya wa kawaida na kuhujumu juhudi zinazoendelea za kupanua upatikanaji wa haki hususan kwa waliotengwa.
Aidha, Koome alitoa wito wa kuwepo njia mwafaka ya kutambua maandamano halali na visa vya uhalifu, akihimiza wahusika wa serikali na wasiokuwa wa serikali kujiunga pamoja kwa haraka na kutafuta suluhu endelevu kwa masuala yanayolikabili taifa.
Alikariri kujitolea kwa idara ya Mahakama katika kutetea haki, hata wakati wa usumbufu na uharibifu.
Mbali na mahakama ya Kikuyu, majengo ya mahakama za Dagoretti na Ol- Kalou ambayo yalikuwa yakitumiwa kuhifadhi vielelezo vya ushahidi pia yalivunjwa na kuharibiwa vibaya.