Martha Karua atangaza kifo cha babake

Alielezea kwamba babake aliaga dunia muda mfupi baada yake na ndugu zake kumtembelea nyumbani katika kaunti ya Kirinyaga.

Marion Bosire
1 Min Read

Kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party, PLP, Martha Karua ametangaza kifo cha babake Mzee Jackson Karua, kilichotokea jana Jumapili.

Kupitia taarifa aliyotoa jana, Martha alielezea kwamba babake aliaga dunia muda mfupi baada yake na ndugu zake kumtembelea nyumbani katika kaunti ya Kirinyaga.

Anasema walikaa na mzee kama wanawe wakamwimbia wimbo aupendao bila kujua kwamba ingekuwa mara ya mwisho kuonana naye akiwa hai. Kiongozi huyo anasema akiwa njiani kurejea Nairobi, alifahamishwa kwamba Mzee ameaga.

Martha anamwomboleza babake kama mzazi aliyemwaminia kuanzia kitambo hata kabla ya kile anachokitaja kuwa mafanikio ya thamani ya kusherehekea.

“Kuanzia siku zangu za shule, miaka yangu katika taaluma ya uanasheria na kupitia sura kadhaa za maisha yangu ya utumishi wa umma, alisalia kuwa mmoja wa walioniunga mkono, alijivunia ufanisi wangu, alikuwa ananitia moyo na kuwa nami,” aliandika Martha.

Mwanasiasa huyo wa upinzani alisema babake alimfunza maadili mema akilalamika kwamba hakuna umri sahihi wa mtu kuwa tayari kuaga mtu ambaye amekuwa kwenye maisha yake kuanzia mwanzo.

Share This Article