Konshens kutumbuiza mashabiki wa Uganda Disemba

Awamu ya pili ya mauzo ya tiketi za tamasha yake imeanza, huku bei zikiongezwa kuelekea siku hiyo.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii maarufu wa muziki wa Dancehall kutoka Jamaica, Konshens, anatarajiwa kurejea nchini Uganda kwa tamasha kubwa itakayofanyika Desemba 11, 2026, katika uwanja wa Lugogo Cricket Oval jijini Kampala.

Tamasha hiyo ya Vibe Republic inayosubiriwa kwa hamu inatarajiwa kuvutia maelfu ya mashabiki wa muziki wa Dancehall wanaotaka kushuhudia burudani ya moja kwa moja kutoka kwa mwanamuziki huyo mashuhuri.

Waandaaji wa hafla hiyo, Talent Africa Group, TAG, wametangaza kuanza kwa awamu ya pili ya mauzo ya tiketi, huku bei zikiongezwa kuelekea siku ya tamasha.

Tiketi ya Citizen Pass sasa inauzwa Shilingi elfu 30 za Uganda kutoka elfu 20 katika awamu ya kwanza. Nayo tiketi ya Diplomat Pass imepanda kutoka elfu 80 hadi elfu 100, pesa za Uganda.

Awamu ya kwanza ya mauzo ya tiketi ilizinduliwa Oktoba 20, 2026, kupitia ofa maalumu iliyolenga kuwapa wanunuzi wa mapema nafasi ya kupata tiketi kwa bei nafuu.

Konshens, ambaye jina lake halisi ni Garfield Spence, anafahamika kupitia nyimbo maarufu za Dancehall zikiwemo “Break Off Yuh Back”, “Gal a Bubble”, “Pull Up to Mi Bumper” na “Do Sumn”.

Msanii huyo ana mashabiki wengi nchini Uganda, ambako maonyesho yake ya awali yameimarisha uhusiano wake na wapenzi wa muziki.

Tamasha hiyo inaandaliwa chini ya chapa ya Vibe Republic, huku Swangz Avenue na Explore Uganda pia zikihusika katika kampeni ya kuitangaza.

Share This Article