Aliyekuwa kiongozi wa genge la uhalifu, Duane “Keffe D” Davis, amehukumiwa kifungo cha miaka 40 hadi maisha jela kwa kupanga mauaji ya mwanamuziki mashuhuri Tupac Shakur mwaka 1996.
Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Clark, Carli Kierny, alitoa hukumu hiyo jana Oktoba 13, 2026, na inajumuisha kifungo cha miaka 20 hadi maisha kwa kosa la mauaji ya daraja la kwanza na miaka 20 hadi maisha kwa kutumia silaha hatari.
Kwa kuwa Davis ana umri wa miaka 63, hukumu hiyo inamaanisha kuwa huenda akafungwa gerezani maisha yake yote, jopo la waamuzi likimkuta na hatia kwa kauli moja Agosti 2026, baada ya majadiliano ya saa tatu pekee.
Chini ya sheria za Nevada, waendesha mashtaka hawakuhitajika kuthibitisha kuwa Davis ndiye alifyatua risasi, bali kwamba alikuwa mtu aliyepanga mauaji hayo na kutoa silaha iliyotumika katika shambulizi la gari lililokuwa likitembea.
Upande wa mashtaka ulitegemea kwa kiasi kikubwa kauli za Davis mwenyewe, ambapo alikuwa akijigamba hadharani kuhusu mauaji hayo kupitia mahojiano kwenye vipindi mbali mbali na kitabu chake cha kumbukumbu alichochapisha mwaka 2019.
Dadake Tupac, Sekyiwa Shakur, alimwelezea msanii huyo kama mtu aliyekuwa akiwalinda wapendwa wake, akisema kifo chake kilivunja familia yao.
Davis hakuonyesha majuto mahakamani, badala yake aliangazia tu kutaka kurejeshewa mali zilizochukuliwa na polisi wakati wa msako wa mwaka 2023.
Mawakili wake wamethibitisha kuwa watakata rufaa kupinga hukumu hiyo.