Mhariri Msaidizi wa shirika la habari la Standard Group, Alex Kiprotich, amepatikana salama baada ya kutekwa nyara katika barabara ya kutoka Gilgil kuelekea Nakuru Jumanne Septemba 1, 2026 usiku.
Kiprotich alipatikana majira ya saa 12 unusu asubuhi leo, karibu na Bwawa la Masinga na kundi la wafanyakazi wa Standard Group likiongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji, Chaacha Mwita.
Mwanahabari huyo aliripotiwa kuachwa na watekaji wake katika eneo hilo saa za mapema za asubuhi.
Kwa mujibu wa Standard Group, Kiprotich alikimbilia nyumba ya familia moja iliyo karibu, ambako alipokelewa na kuhudumiwa. Yuko salama, ingawa bado ameshtushwa na tukio hilo.
Kampuni hiyo ya habari inawashukuru wote walioshiriki katika msako wa usiku kucha, waliotoa maombi na kuunga mkono familia na wenzake Kiprotich.
Hali iliyosababisha kutekwa kwake bado haijafahamika kikamilifu na imezua wasiwasi miongoni mwa wanahabari. Standard Group imesema itaendelea kushinikiza uwajibikaji kamili na kutoa taarifa zaidi kadri zitakavyopatikana.
Kwa sasa, kampuni hiyo imesema jambo muhimu zaidi ni kwamba Kiprotich yuko salama baada ya tukio hilo la kutisha.