Kindiki: Bidhaa za Kenya kuingia China bila kutozwa ushuru

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na Makamu wa Rais wa China Han Zheng.

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amesema uhusiano ulioimarika kati ya Kenya na China, umefanikisha bidhaa za Kenya kuingia katika soko la China bila kutozwa ushuru.

Kindiki alidokeza kuwa Kahawa, Majani Chai, Mboga, Matunda, Maua na Madini, zitaingia kwenye soko la China bila kutozwa ushuru, hatua itakayowafaidi kiuchumi mamilioni ya wakulima na wafanyabiashara wa Kenya pamoja na kampuni za usafirishaji bidhaa nje ya nchi.

“Pengo kati yetu na mataifa yaliyostawi ni utajiri, na njia mwafaka ya kubuni utajiri ni kupitia biashara,” alisema Prof. Kindiki.

Alisema lengo la Kenya la kuwa taifa lililostawi linazidi kuafikiwa hatua kwa hatua.

Naibu huyo wa Rais aliyasema hayo Jumatatu akiwa ameandamana na Makamu wa Rais wa China anayezuru hapa nchini Han Zheng, walipozindua shehena ya kwanza iliyokuwa na bidhaa za Kenya ikielekea nchini China bila kutozwa ushuru.

Weingine walioshuhudia hafla hiyo ni pamoja na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Ustawi wa Viwanda Lee Kinyanjui, Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir, na Makatibu wa Wizara mbalimbali pamoja na maafisa wa ngazi za juu serikalini.

Share This Article