Kifo cha Ngugi wa Thiongo, pigo kwa tasnia

Ngugi alipata umaarufu kwa kitabu cha Weep Not, Child cha mwaka 1964, akiwa mwandishi wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kuandika riwaya.

Dismas Otuke
2 Min Read

Mwandishi mashuhuri wa vitabu Ngũgĩ wa Thiong’o, aliaga dunia Jumatano usiku akiwa na umri wa miaka 87.

Kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya uandishi wa vitabu kutokana na mchango wake mkubwa, ikiwemo kufichua uozo katika jamii.

Ngugi alijulikana sio tu Kenya, bali pia bara zima la Afrika kwa uandishi wake maridhiwa uliodumu kwa miongo kadhaa katika lugha za Kiingereza na Kikuyu.

Hadi kifo chake, marehemu alikuwa ameandika riwaya na michezo ya kuigiza sio haba kuhusu unywaji pombe kupindukia, changamoto za Kenya baada ya kujipatia uhuru, tamaduni na lugha za jamii za Kiafrika.

Ngugi alipata umaarufu kwa kitabu cha Weep Not, Child cha mwaka 1964, akiwa mwandishi wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kuandika riwaya.

Baadaye aliandika riwaya ya River Between mwaka 1965 na Petals of Blood, mwaka 1965, kilichomtia mashakani kutokana na kufichua uozo serikalini kama vile ufisadi, usaliti, na kukosa usawa serikalini.

Riwaya hiyo ilipigwa marufuku na serikali.

Baadaye aliandika kitabu cha kuigiza cha Ngaahika Ndeenda (I Will Marry When I Want), kwa lugha ya Kikuyu.

Mchezo huo ulikashifu maovu na dhuluma za serikali kwa jamii, kilichosababisha kukamatwa na kufungwa gerezani na serikali.

Alipotoka gerezani miaka ya 80, Ngugi aliendelea kuhangaishwa na serikali na kuhiari  kutorokea Marekani.

Mwaka 2020 kitabu chake cha The Perfect Nine, kinachoelezea chimbuko la kabila ya Kikuyu, kiliteuliwa kuwania tuzo ya kimataifa.

Mola ailaze roho yake mahali pema penye wema.

Website |  + posts
Share This Article