Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amesema Kenya inaimarisha ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa, UN na washirika wengine ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 utakuwa na uwazi, wa kuaminika, huru, wa usawa na wenye amani.
Mudavadi ameyasema hayo leo Jumatatu alipokutana na mshauri mkuu wa uchaguzi wa kitengo cha Afrika Mashariki chini ya Misheni ya Tathmini ya Mahitaji ya Umoja wa Mataifa (NAM), Akinyemi Adegbola aliyemtembelea akiwa na ujumbe wake.
Mudavadi akiusifia mkutano huo alioutaja kama hatua muhimu katika kuimarisha asasi za kidemokrasia na kulinda uadilifu wa michakato ya uchaguzi nchini.
“Niliunga mkono wajibu wao usiokuwa na upendeleo wa kutathmini mandhari ya kisiasa na uchaguzi nchini Kenya na katika kutoa mapendekezo juu ya namna UN inaweza kusaidia ipasavyo safari yetu ya uchaguzi,” alisema Mudavadi.
“Kama serikali, tumedhamiria kuhakikisha kila uchaguzi unaakisi matamanio ya raia, wakati tukiheshimu uhuru wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC,” aliongeza Mkuu huyo wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.
Kauli zake zinawadia wakati ambapo IEBC inajibidiisha kusajili wapiga kura wapya kupitia shughuli endelevu ya usajili wa wapiga kura nchini.
Ingawa tume hiyo inasema inalenga kuadikisha hadi wapiga kura milioni 28.5, ni idadi ndogo ya Wakenya ambao wamekuwa wakijitokeza kujiandikisha kama wapiga kura tangu kuzinduliwa kwa shughuli hiyo Septemba 29 mwaka huu.
Rais William Ruto amewaongoza viongozi wengine wa kisiasa kuwarai Wakenya hasa vijana kujitokeza na kujiandikisha kama wapiga kura kwani kura ndio itakayokuwa silaha yao madhubuti ya kuamua uongozi wautakao kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.