Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA Tundu Lissu amefikwa na msiba baada ya kakake ambaye pia ni wakili Allute Lissu Mughwai, kufariki.
Kulingana na taarifa, Allute aliaga dunia saa 8 usiku wa kuamkia leo, Novemba 1, 2026, wakati akipatiwa matibabu hospitalini Jijini Arusha.
Dadake marehemu kwa jina Rose Masesa alithibitisha habari hizo akielezea kwamba kakake alikuwa akiugua kwa muda mrefu, lakini hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri hadi juzi, kiasi kwamba familia ilitarajia angesafiri kwenda Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Masesa, hali ya Allute ilibadilika ghafla na akakimbizwa hospitalini ambako alifariki dunia.
“Alizidiwa ghafla, akakimbizwa hospitali, alikuwa anaumwa muda mrefu, lakini hii ya kuzidiwa imetushtua sana na alikuwa anaendelea vizuri na tulijua anakuja Dar, tunamshukuru Mungu,” alisema Masesa.
Aidha, ameeleza kuwa Wakili Allute amefariki dunia katika Hospitali ya Siriani, Jijini Arusha na kwamba msiba kwa sasa upo nyumbani kwa Marehemu jijini humo, huku akibainisha kuwa hadi sasa hakuna ratiba rasmi ya mazishi iliyotolewa.
Tundu Lissu amekuwa kizuizini kwa muda mrefu akikabiliwa na mashtaka ya uhaini. Kesi yake imefikia hatua yake kusomewa hukumu shughuli inayopangwa kufanyika Novemba 6, 2026.
