Diamond aahidi kushirikiana na msanii wa Uganda

Akizungumza na wanahabari jijini Kampala Diamond alisema amerekodi nyimbo na wasanii wengi wa Uganda awali lakini hazijafanikiwa kutoka.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz, ametangaza mipango ya kutoa wimbo wa ushirikiano na msanii kutoka Uganda hivi karibuni, baada ya majaribio kadhaa ya awali kushindikana.

Mwimbaji huyo, aliyewasili Uganda Alhamisi kabla ya kutumbuiza, alisema anatarajia kutoa wimbo akishirikiana na msanii wa Uganda mwakani au hata kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari jijini Kampala Alhamisi jioni, Diamond alisema amerekodi nyimbo na wasanii wengi zaidi wa Uganda kuliko wasanii kutoka nchi nyingine yoyote duniani.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na tetesi kuhusu ushirikiano wake na wasanii mbalimbali wakiwemo Spice Diana, Fik Fameica na Gloria Bugie, lakini miradi hiyo haijawahi kutolewa rasmi.

Diamond alisema kila mara wamekuwa wakikumbana na changamoto zinazozuia nyimbo hizo kutoka, akiamini kuwa huenda ni mipango ya Mungu.

Alieleza kuwa huenda Mungu anaandaa ushirikiano mkubwa utakaotamba katika vituo vya redio duniani kote.

“Kwa kweli, ni suala la Mungu na muda mwafaka. Nimefanya nyimbo nyingi na wasanii mbalimbali kutoka hapa Uganda kuliko nilizofanya na wasanii wa nchi nyingine yoyote. Kwa bahati mbaya, hakuna hata mmoja uliotolewa. Hakuna anayepaswa kumlaumu mwenzake kwa sababu ni suala la muda,” alisema.

Aliongeza kuwa Tanzania na Uganda zina historia nzuri ya kimuziki na huenda ushirikiano huo ukazaa wimbo mkubwa utakaovuka mipaka.

Share This Article