Naibu Rais Prof. kithure kindiki ametoa wito kwa Idara ya Mahakama kukabiliana na ufisadi na kuzingatia maadili inapotatua migogoro, kwa manufaa ya udhabiti wa taifa hili.
Kindiki wakati huo huo, aliwataka majaji na maafisa wa Idara ya Mahakama kuongeza bidii, ili kufanikisha jukumu muhimu la idara hiyo.
Hata hivyo, aliipongeza mahakama kwa kushughulikia ipasavyo mrundiko wa kesi kupitia mfumo wa dijitali na kuwaajiri maafisa zaidi, akikiri kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazopaswa kushughulikiwa.
Huku akiipigia debe serikali, Kindiki alisema utawala wa Rais William Ruto umewaajiri majaji wengi, na kuongeza mgao kwa Idara ya mahakama kutoka shilingi bilioni 18 mwaka 2022, hadi shilingi bilioni 30 mwaka huu.
“Tumefanikisha uidhinishaji wa sheria ya kustaafu kwa Majaji na kuisaida Idara ya Mahakama kupata hati za kumiliki ardhi iliyonyakuliwa kutoka kwake,” alisema kindiki.
Kindiki aliyasema hayo leo Ijumaa, kwenye hafla ya uzinduzi wa ripoti kuhusu hali ya Idara ya Mahakama na Utekelezaji wa Haki, iliyoandaliwa katika Mahakama ya Upeno, Jijini Nairobi.