DPP aidhinisha mashtaka ya mauaji kwa bintiye Regina Re

Anapendekeza kwamba Thandie Malaika Wanjiku Gitao, awajibishwe kwa mauaji ya nyanyake, wa miaka 86, Dorita Lasinder Macharia.

Marion Bosire
1 Min Read

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP, ameidhinisha kufunguliwa kwa mashtaka ya mauaji dhidi ya Thandie Malaika Wanjiku Gitao.

Thandie ni binti ya aliyekuwa mwigizaji wa televisheni Regina Wambui Gitao, maarufu kama Regina Re, na mashtaka hayo yanahusiana na kifo cha nyanyake wa miaka 86, Dorita Lasinder Macharia.

Thandie atakabiliwa na shtaka la mauaji kinyume na Kifungu cha 203 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 204 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Aidha, Regina na kaka yake Alton Jimmy Macharia watashtakiwa kwa kusaidia kuficha uhalifu baada ya mauaji, kinyume na Kifungu cha 222 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 396(1) cha sheria hiyo.

Wawili hao wanadaiwa kuingilia eneo la tukio kwa lengo la kuficha ushahidi na kufunika madai ya kuhusika kwa Thandie katika mauaji hayo.

Watatu hao wanatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkuu wa Kibera kesho Jumatano, Novemba 18, 2026, kujibu mashtaka.

Uchunguzi wa maiti uliofanywa Novemba 3, 2026, ulibaini kuwa Dorita alifariki kutokana na kupoteza damu nyingi kufuatia majeraha kadhaa yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali, yakiwemo majeraha usoni, shingoni na kukatwa kwa mishipa ya damu.

Sababu ya kifo ilirekodiwa kuwa kupoteza damu nyingi kutokana na jeraha la kuchomwa shingoni lililosababisha kuharibika kwa mishipa ya damu.

Share This Article