Mwanawe Rais wa Uganda ambaye pia ni mkuu wa majeshi ya Uganda Muhoozi Kainerugaba amesema tena kwamba atawania urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2031.
Katika ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wa X Jumanne, Novemba 17, Kainerugaba alisema anatarajia kuwania wadhifa huo baada ya Museveni, akisisitiza kuwa hakuna mtu atakayemzuia kutimiza azma yake.
“Nitagombea urais wa nchi hii baada ya Mzee. Hakuna atakayenizuia. Ninaweka matumaini yangu kwa Mwenyezi Mungu na wananchi wenzangu, wanaume na wanawake,” aliandika.
Tamko hilo limeibua tena mjadala kuhusu mustakabali wa uongozi wa Uganda, kufuatia tangazo lake la Agosti mwaka huu kwamba alikusudia kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2031.
Wakati huo, Jenerali huyo mwenye umri wa miaka 52 alieleza matumaini ya kushinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 90 ya kura, akitegemea pia uungwaji mkono wa babake.
Kainerugaba, ambaye anaongoza kundi la kisiasa la Patriotic League of Uganda, aliwahi kuonyesha nia ya kuwania urais katika uchaguzi wa Januari 2026 kabla ya kujiondoa.
Museveni, wa miaka 81, amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 na alishinda muhula wa saba Januari 2026. Hata hivyo, bado haijafahamika iwapo atawania muhula mwingine katika uchaguzi wa 2031.