Kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua ameelezea imani kwamba chama hicho kitashinda viti vyote katika kaunti ya Nairobi kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza wakati akifungua ofisi ya DCP jijini Nairobi leo Jumatatu, Gachagua pia amepuuzilia mbali kura ya maoni ya hivi karibuni iliyoashiria chama cha ODM ndicho maarufu zaidi katika kaunti ya Nairobi.
“Chama hiki kitapata kura zote milioni 2.7 hapa Nairobi,” alisema Naibu huyo wa zamani wa Rais wakati akidai kuwa DCP ndicho chama kinachowika Nairobi.
Kaunti ya Nairobi ina maeneo bunge 17 na wadi 85.
Gachagua anasema chama chake kiko tayari kuwabwaga wapinzani wake ikiwa ni pamoja na ODM na UDA katika uchaguzi mkuu utakaoandaliwa Agosti 10 mwakani.
Aidha, amewahakikishia wagombea wote kwa tiketi ya chama hicho kuwa uchaguzi wa mchujo utakuwa huru na wa usawa.
Amesema kamwe hatakubali kuvurugwa kwa uchaguzi wa mchujo kunakoweza kuleta migawanyiko chamani na pia kutoa hakikisho kuwa hakuna mgombea anayependelewa.