Kapeke asema ugomvi husaidia wasanii kukua

Alisema ushindani huwapa wasanii motisha wa kufanya kazi kwa bidii, kuboresha ubunifu wao na kuthibitisha uwezo wao.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii wa muziki nchini Uganda Kapeke ametetea ushindani na mivutano kati ya wasanii akisema vinaweza kusaidia wanamuziki kukuza vipaji vyao, kuimarisha taaluma zao na kuvutia mashabiki wengi zaidi.

Akizungumzia sekta ya muziki, Kapeke alisema ushindani huwapa wasanii motisha wa kufanya kazi kwa bidii, kuboresha ubunifu wao na kuthibitisha uwezo wao.

Alieleza kuwa hatua zinazochukuliwa na msanii mmoja mara nyingi huchochea wengine kuiga au kufanya vizuri zaidi, hali inayochangia ukuaji wa tasnia nzima.

“Kapeke anapofanya jambo, mtu mwingine pia hutaka kulifanya,” alisema.

Mwimbaji huyo amezungumzia pia suala la usimamizi wa wasanii, akisema yeye hahitaji kuwa na timu ya usimamizi wa kazi yake ya muziki kwa sasa, akisisitiza kuwa ana uwezo wa kuendesha taaluma yake mwenyewe.

Akizungumza kwenye mahojiano, Kapeke alisema nyimbo zake hupigwa kwenye vituo vya redio, hutengeneza video za muziki mara kwa mara, ana mashabiki na huzingatia muda wa maonyesho anayopangiwa.

Alisema umuhimu wa kuwa na usimamizi, hutegemea hatua ambayo msanii amefikia katika taaluma yake, akiongeza kuwa baadhi ya wanamuziki wanahitaji msaada huo lakini yeye hana haraka ya kuwa na meneja.

“Najua muziki na najua cha kufanya,” alisema.

Share This Article