PPMC yaandaa warsha kwa mameneja wa wanamuziki

Mkutano huo wa kesho uko wazi kwa mameneja wote wa wanamuziki na muziki wanaofanya kazi hiyo na wanaotaka kuingia katika sekta hiyo.

Marion Bosire
1 Min Read

Tume ya Kudumu ya Rais kuhusu Muziki Nchini Kenya, PPMC, imewaita mameneja wote wa wanamuziki kwa ajili ya warsha ya saa tatu.

Lengo kuu la mkutano huo ni kuwapa wasimamizi hao wa muziki ujuzi wa kujenga chapa imara na endelevu za wasanii.

Warsha hiyo itafanyika kesho Jumatano, Septemba 30, katika ofisi za PPMC zilizoko barabara ya State House, kuanzia saa 6 mchana hadi saa 9 alasiri.

Warsha hiyo itaendeshwa na Mike Mutenyo, anayefahamika kwa jina la “The Brand Guru” na itajikita katika misingi ya kujenga chapa zinazovutia hadhira, kuongeza mauzo na kudumu kwa muda mrefu.

Warsha hiyo iko wazi kwa mameneja wote wa wanamuziki na muziki ambao tayari wanafanya kazi hiyo pamoja na wale wanaotaka kuingia katika sekta hiyo.

Kushiriki ni bure bila malipo na washiriki wanakaribishwa kufika moja kwa moja, kujisajili na kushiriki.

PPMC ilianzishwa mwaka 1988 kama tume ya serikali yenye jukumu la kuendeleza muziki na ngoma za kitamaduni, kusaidia maendeleo ya tasnia ya muziki nchini Kenya, pamoja na kuhifadhi sanaa na maonyesho ya muziki ya Kenya.

Mwaka 2008, Tume hiyo ilibadilishwa kuwa Idara ya Muziki chini ya Wizara ya Nchi ya Urithi wa Kitaifa na Utamaduni.

Share This Article