Msanii wa muziki nchini Tanzania Faustina Charles Mfinanga, maarufu kama Nandy, ametoa shukurani za dhati wa wote waliohusika katika kufanikisha tamasha yake ya mwaka huu.
Huku akijipongeza yeye na wenzake kwa miaka mitano ya bidii bila kuchoka, Nandy alionekana kutangaza mwisho wa awamu ya mwaka 2026 wa tamasha yake akisema, “Hii ni Nandy Festival 2026 tunaondoka,”.
Alielekeza ujumbe wake wa shukrani kwa watu wote ambao walimshika mkono tangia mwanzo mpaka sasa, wakati ambapo anasema anafanya tamasha hiyo kwa ukubwa wa kimataifa.
“Shukrani kwa mashabiki wetu duniani kote kwa usaidizi wenu una maana kubwa sana kwetu,” aliandika msanii huyo.
Kwa msimamizi wake wa tamasha aitwaye Majizzo, Nandy alimsifia akisema kwamba ametisha mno kwa kufanya maandalizi kwa kiwango cha kimataifa akiongeza, “Umekuja uweka alama kubwa sana kwenye tasnia yetu!”
Msanii huyo hakusahau waandishi wa habari wa vyombo vya habari na wa mtandaoni aliowataja kuwa wanafamilia ambao wametoa msaada wa maana kwa Nandy Festival.
“Mwisho kabisa kundi langu, ebanaa bado kidogooooo tu yaaani kidogooo tu tunafika tuendelee kusukuma! Nawapenda,” alimalizia msanii huyo.
Nandy alianzisha Nandy Festival mwaka 2019 ambapo anazunguka katika mikoa tofauti nchini Tanzania kutumbuiza na amefanikiwa kuwa na awamu tano zikiwemo za miaka 2021, 2022, 2024 na 2026.