Kenya na Zimbabwe zatia saini Mikataba saba ya Maelewano

Rais William Ruto alisema miongoni mwa mikataba hiyo ni ile ya nyumba nafuu na utoaji wa vifaa vya ujenzi na teknolojia.

Tom Mathinji
1 Min Read
Kenya na Zimbabwe zatia saini Mikataba saba ya Maelewano.

Kenya na Zimbabwe leo Ijumaa zimetia saini Mikataba saba za Maelewano zinazolenga kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Hafla hiyo iliongozwa na Rais William Ruto na mgeni wake Emmerson Mnangagwa katika Ikulu ya Nairobi.

Kupitia kwa taarifa Rais William Ruto alisema miongoni mwa mikataba hiyo ni ile ya nyumba nafuu na utoaji wa vifaa vya ujenzi na teknolojia.

“Ushirikiano huu utafanikisha ubadilishanaji wa utaalam na teknolojia katika nyumba za bei nafuu, mojawepo wa mipango yenye mageuzi makubwa nchini Kenya,” alisema Rais Ruto.

Ili kuimarisha biashara na mauzo ya nje  kati ya nchi hizo mbili, Ruto alisema mataifa hayo mawili yalitia saini mkataba  kuhusu biashara na forodha.

Mikataba mingine ni katika sekta ya habari na mawasiliano ambapo Shirika la Habari la Kenya (KNA) na Shirika la Habari la Zimbabwe (ZIANA) zitabadilishana maudhui ya habari.

Nchi hizo mbili pia zilitia saini mkataba Mambo ya Nje, ushirikiano wa sanaa, utamaduni na turathi, pamoja na mkataba kuhusu sheria na usalama.

“Tulikariri kujitolea kwetu kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kupanua biashara na uwekezaji,” alisema Rais Ruto.

Rais Mnangagwa yuko nchini Kenya kwa ziara rasmi ya siku mbili.

Share This Article