Ruto: Mfumo mpya wa ufadhili ndio suluhu kwa maendeleo ya Afrika

Rais ametoa wito kwa bara la Afrika kuunga mkono na kustawisha taasisi zake lenyewe.

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto amesema mfumo mpya wa ufadhili barani Afrika unahitajika kwani hiyo ndio suluhu mujarabu katika kuchochea maendeleo barani humo. 

“Ni wakati wa kuunga mkono taasisi zetu wenyewe, kuziimarisha na kuzipa uwezo wa kifedha wa kukusanya mtaji, kuzuia hatari na kuchochea ustawi wa bara hilo kwa masharti ya Afrika,” amesema Rais Ruto.

“Lengo ni kuiondoa Afrika kutoka kuwa mpokeaji wa mtaji wa dunia hadi kuwa mkusanyaji wa mtaji wake yenyewe na kutoka kwa utegemezi wa tathmini ya hatari kutoka nje hadi kuwa taasisi za Kiafrika zenye uwezo wa kubaini fursa zilizopo Afrika kwa usahihi.”

Rais Ruto aliyasema hayo alipokuwa mwenyeji wa dhifa ya Mkutano Mkuu wa Kila Mwaka wa 26 wa Biashara na Bima ya Maendeleo ya Uwekezaji barani Afrika (ATIDI) katika Ikulu ya Nairobi.

Aliongeza kuwa Kenya tayari inaongoza katika hilo akitoa mfano wa Mfuko wa Miundombinu ya Kitaifa ambao unatumiwa kukusanya fedha humu nchini kwa kiwango ambacho alisema hakijawahi kushuhudiwa.

“Kufikia mwisho wa wiki hii, mfuko huo utakuwa umekusanya shilingi bilioni 300 ambazo ni sawa na dola bilioni 2.3 ambazo zikitumiwa kwa uwiano wa 1:10, zitatumiwa kufadhili miundombinu mikubwa ya maendeleo,” aliongeza Rais.

Share This Article