Operesheni iliyoongozwa na taarifa za kijasusi iliyofanywa jana na maafisa wa upelelezi eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, ilisababisha kukamatwa kwa mshukiwa mmoja wa wizi.
Jamaa huyo anayehusishwa na visa kadhaa vya wizi wa kimabavu na uvamizi wa nyumba, alikamatwa pamoja na watu wengine wawili wanaoshukiwa kupokea au kuhifadhi mali zilizoibwa.
Operesheni hiyo pia iliwezesha kupatikana kwa bidhaa mbalimbali zinazoshukiwa kuibwa, ikiwemo mitungi 17 ya gesi, majiko saba ya gesi, vishikio 17 vya mitungi ya gesi, pamoja na simu za rununu na vifaa vyake.
Washukiwa hao watatu walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Likoni, ambako wamezuiliwa huku polisi wakisubiri kuchukua hatua zaidi, wakati uchunguzi ukiendelea.
Huduma ya Kitaifa ya Polisi imesema itaendelea kuwafuatilia wote wanaohusishwa na mitandao ya uhalifu na kuimarisha usalama katika jamii.
Polisi wamewataka wananchi kuendelea kushirikiana na maafisa wa usalama na kutoa taarifa zozote zinazoweza kusaidia kudumisha amani na utulivu.