Wabunge wameibua wasiwasi kuhusu mrundiko wa madeni katika Ofisi ya Naibu Rais, wakitaka maelezo kuhusu matumizi ya fedha za umma na tofauti katika takwimu za madeni zilizowasilishwa na taasisi mbalimbali za serikali.
Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Utawala na Usalama wa Ndani iliibua masuala hayo leo Jumanne ikichunguza mapendekezo ya bajeti ya ofisi hiyo chini ya Taarifa ya Sera ya Bajeti ya mwaka 2027.
Mbunge wa Loima, Protus Akuja, alitaka ufafanuzi kuhusu tofauti ya takwimu za madeni ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026.
Ofisi ya Naibu Rais iliripoti madeni ya shilingi milioni 552.6, huku ripoti ya sekta ya Utawala wa Umma na Mahusiano ya Kimataifa ikionyesha milioni 569.8.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gabriel Tongoyo, alitaka kujua ni kwa nini madeni yanaendelea kuongezeka licha ya kulipwa mwanzo kila fedha zinapotolewa.
Alionya kuwa huenda baadhi ya matumizi yalifanywa bila kutengewa fedha katika bajeti iliyoidhinishwa.
Afisa Mkuu wa Fedha wa ofisi hiyo alisema madeni yanapatiwa kipaumbele katika matumizi ya fedha zinazopatikana.
Hata hivyo, alifichua kuwa deni lililokuwa limebaki limepungua hadi takriban shilingi milioni 150, huku gharama za ukarimu zikichangia sehemu kubwa.
Maafisa hao pia walisema ofisi iliomba shilingi bilioni 7 lakini inatarajia kupokea takriban shilingi bilioni 4 , hali inayoweza kuathiri shughuli zake.
Katibu Mkuu wa Utawala, Moses Mbaruku, alihusisha shinikizo la matumizi na madeni yaliyosalia na majukumu ya kikatiba ya Naibu Rais.
Kamati pia ilihoji matumizi ya fedha za maandalizi ya athari za mvua ya El Niño na kuchelewa kwa ukarabati wa makazi ya Karen na Mombasa, miradi iliyotengewa milioni 70.