Namna uhusiano kati ya Kenya na DRC ulizorota

Uhusiano huo uliharibika vibaya mwezi Desemba mwaka 2023 kufuatia kutokubaliana kuhusu mzozo wa mashariki mwa DRC.

Marion Bosire
2 Min Read
Marais William Ruto, Felix Tshisekedi na Dennis Nguesso katika mkutano wa ngazi za juu mjini Oyo nchini Congo jana

Taarifa kuu leo nchini Kenya ni kuhusu mkutano wa ngazi za juu ulioandaliwa kati ya Marais wanne mjini Oyo katika Jamhuri ya Congo uliolenga kuhuisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili. 

Lakini huenda wengi wasifahamu namna uhusiano huo uliharibika na kufikia kiwango cha kutatuliwa na Umoja wa Afrika, AU kupitia Rais wa Togo Faure Essozimna Gnassingbé ambaye ni mpatanishi.

Rais Denis Sassou N’Guesso wa Congo naye alitoa mahali pa mkutano huo kufanyika.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ulifikia kiwango cha chini zaidi mwezi Desemba mwaka 2023 kufuatia kutokubaliana kuhusu mzozo wa mashariki mwa DRC.

Mvutano ulianza mapema mwaka huo kutokana na tofauti kuhusu jukumu la kikosi cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichoongozwa na Kenya na kutumwa mashariki mwa DRC.

Wakati Kinshasa ilitarajia wanajeshi hao kufanya operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa M23, kikosi hicho kilikuwa na jukumu la kujihami.

Hali hiyo ilimfanya Rais Félix Tshisekedi kukataa kuongeza muda wa kikosi hicho, kilichoondolewa nchini humo mwezi Desemba mwaka 2023.

Hali ilizidi kuwa mbaya Desemba 15, 2023, baada ya aliyekuwa mkuu wa tume ya uchaguzi nchini DRC, Corneille Nangaa, kuzindua muungano wa Congo River mjini Nairobi, muungano uliohusishwa na waasi wa M23.

Kinshasa ilipinga uamuzi wa Kenya wa kutowakamata waandaaji wa mkutano wa viongozi wa muungano huo, huku Rais William Ruto akitetea msimamo huo kwa hoja ya uhuru wa kujieleza.

DRC ilimwita balozi wake kutoka Nairobi, huku waandamanaji wakiharibu ubalozi wa Kenya mjini Kinshasa.

Mvutano mwingine uliibuka mwezi Agosti mwaka 2025 baada ya Kenya kumteua afisa wa ubalozi wa mjini Goma bila idhini ya Kinshasa.

Hata hivyo, jana Jumapili, Novemba 22, 2026, Rais Ruto na Tshisekedi walikubaliana kurejesha uhusiano kamili wa kidiplomasia katika mkutano uliofanyika mjini Oyo katika Jamhuri ya Congo.

Share This Article