Wazee wa Isiolo walalamikia mvutano mpakani

Wawakilishi wa jamii za Borana, Gabra na Sakuye walionya kuwa ghasia zinaweza kuharibu uhusiano wa muda mrefu kati ya jamii za eneo hilo.

Marion Bosire
2 Min Read

Wazee wa kaunti ya Isiolo wamelalamikia ongezeko la mvutano kwenye mpaka wa kaunti za Garissa na Isiolo kufuatia vurugu zilizoshuhudiwa eneo la Janju na kusababisha vifo vya watu 9.

Wakizungumza na wanahabari mjini Isiolo, wawakilishi wa mabaraza ya wazee wa jamii za Borana, Gabra na Sakuye walionya kuwa ghasia zinaweza kuharibu uhusiano wa muda mrefu kati ya jamii za Borana na Somali.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Borana, Abduba Nagele, mzee wa jamii ya Gabra Guyo Tuke na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Sakuye, Isaack Kara, viongozi hao waliwataka wakazi kujizuia na kukataa mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Katika taarifa, wazee hao walielezea wasiwasi kuhusu ripoti za mipango ya mashambulizi ya kulipiza kisasi yanayolenga maeneo ya Kinna na Modogashe Kaunti Ndogo ya Garbatula.

Waliitaka Idara ya Ujasusi, Idara ya Upelelezi wa Jinai na mashirika mengine ya usalama kuimarisha ukusanyaji wa taarifa za kijasusi ili kuzuia ghasia zaidi.

Aidha, wazee hao walionya wanasiasa dhidi ya kutoa matamshi ya uchochezi, wakisema yanaweza kuzidisha hali ya taharuki.

Kara alikanusha madai kwamba jamii fulani inahifadhi wanamgambo wa Oromo, akiyataja kuwa uongo na yanaweza kuleta madhara.

Viongozi hao waliitaka serikali kuongeza doria, kulinda wakazi na mali zao na kuhakikisha wahusika wa mauaji wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Share This Article