Polisi Uganda wafafanua kumzuia King Saha kutumbuiza Nyege Nyege

Yeye na msafara wake walizuiwa kuingia eneo la tamasha baada ya kukataa kufanyiwa ukaguzi wa lazima wa kiusalama.

Marion Bosire
1 Min Read
King Saha

Maafisa wa Polisi nchini Uganda wametoa taarifa kuelezea mazingira yaliyosababisha mwanamuziki King Saha kukosa kutumbuiza kwenye tamasha ya Nyege Nyege mwaka 2026.

Wanasema yeye na msafara wake walizuiwa kuingia katika eneo la tamasha baada ya kudaiwa kukataa kufanyiwa ukaguzi wa lazima wa kiusalama.

Katika taarifa hiyo polisi walisema King Saha aliwasili katika kituo cha ukaguzi wa usalama usiku wa manane, Novemba 21, akiwa ameandamana na watu wapatao 30 wanaodaiwa kuwa sehemu ya timu yake.

Kwa mujibu wa polisi, kundi hilo lilikataa kufuata taratibu za lazima za ukaguzi wa kiusalama, hali iliyosababisha maafisa wa usalama kuwanyima ruhusa ya kuingia katika eneo la tamasha kufuatia mzozo mfupi.

Polisi walidai kuwa kundi hilo lilisisitiza kuwa linapaswa kupatiwa msamaha wa ukaguzi kutokana na umaarufu wao, licha ya kuambiwa kuwa masharti ya kiusalama yalitumika kwa kila mtu bila ubaguzi.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa King Saha hatimaye aliwaagiza washiriki wa timu yake kuondoka katika kituo hicho cha ukaguzi, na wakaondoka bila kuruhusiwa kuingia katika eneo la tamasha.

Tukio hilo linajiri baada ya taarifa za kutokubaliana kati ya timu ya King Saha na maafisa wa usalama wa tamasha, hali iliyosababisha mwanamuziki huyo kukosa nafasi yake iliyopangwa ya kutumbuiza.

Share This Article