Mwigizaji wa Kenya, Gloria Moraa, anasherehekea siku yake ya kuzaliwa leo Septemba 20, 2026, ambapo ametimiza umri mpya wa miaka 42.
Mrembo huyo amechapisha ujumbe mzito wa kibinafsikwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, unaoangazia changamoto zake, ustahimilivu, na matumaini mapya ya siku zijazo.
Katika chapisho hilo, Moraa alifichua kuwa kuna wakati ambapo hakutegemea kuishi hadi kufikia miaka 42, akisema alikuwa amefikia hatua ambayo alitamani “kukata pumzi ya mwisho.”
Hata hivyo, mwigizaji huyo aliwashukuru marafiki wa karibu na wanafamilia kwa kumuunga mkono katika nyakati ngumu, huku akikiri kwamba pia amekutana na watu waliomtakia msongo wa mawazo na hata kifo.
“Uzuri ni kwamba Mungu hatoki katika kijiji cha mtu yeyote,” Moraa aliandika, akionyesha imani yake na msimamo kwamba Mungu ameendelea kumstawisha.
Anapoanza mwaka wake wa 42, Moraa alisema anapokea maisha kwa mtazamo chanya na msisimko kuhusu yaliyo mbele yake. Alijieleza kama mtu mwenye “hamasa, mkali, mchangamfu, aliyekamilika, mcheshi, mwenye msimamo, mwepesi na mwenye kasi,” akionyesha nia yake ya kukabiliana na sura hii mpya kwa nguvu na madhumuni.
Moraa pia alimsifu Mungu kwa kumpa nguvu alizosema hawezi kuzielezea, akithibitisha tena imani na shukrani zake.
Alihitimisha ujumbe huo kwa kujitakia neema ya Mungu, upendo, furaha, nguvu, na amani, akitangaza kwamba yuko tayari kwa umri wa miaka 42. “42 niko tayari sana kwa ajili yako,” aliandika.