Ripoti zilizoibuka awali kwamba mwanamuziki Kanye West na mpenzi wake Bianca Censori waliondolewa kwa lazima kutoka eneo la utoaji wa tuzo za Grammy sio za kweli.
Mmoja wa wahudumu wa hafla hiyo amethibitisha kwamba Kanye alikuwa amealikwa kwa hafla hiyo na alikuwa ameteuliwa kuwania tuzo katika kitengo cha wimbo bora wa mtindo wa Rap.
Kanye na Bianca walishangaza wengi kwenye ‘red carpet’ ya Grammys baada ya Bianca kuamua kuvua koti kubwa la rangi nyeusi alilokuwa amevaa na kubakia na kinguo kidogo kinachoonyesha mwili cha rangi inayofanana na ngozi yake.
Wengi walidhania kwamba alibakia uchi na hatua yao ya kuondoka mapema ikasababisha minong’ono kwamba huenda walilazimishwa waondoke na walinzi.
Wahudumu hata hivyo wamesema kwamba wawili hao waliingia kwa hiari na wakatoka kwa hiari na kwamba maafisa wa polisi na wahudumu wengine wa ulinzi hawakuhusika kabisa.
Polisi walidhibitisha pia kwamba hakuna yeyote aliyekuwa amelalamika kuhusu wawili hao.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Kanye kuhudhuria tuzo za Grammy tangu mwaka 2015 na wengi hawakutarajia kumwona huko hasa baada ya matamshi yake ya mwaka 2022.
Wakati huo alizungumza maneno mengi dhidi ya wayahudi lakini baadaye aliomba msamaha.