Awamu ya nne ya tuzo za Sanaa na Burudani barani Afrika yaani Africa Arts Entertainment Awards itaandaliwa jijini Nairobi mwaka huu.
Wasanii mbali mbali wa Kenya wameteuliwa kuwania tuzo katika vitengo mbali mbali vya tuzo hizo zitakazotolewa Machi 30, 2025.
Nadia Mukami ameteuliwa kuwania tuzo kwenye vitengo vitano ambavyo ni Albamu ya studioni ya mwaka mara mbili kwa kazi zake Kenya na Queen of The East, video bora ya muziki ya mwaka, msanii bora wa kike wa mwaka na kazi bora ya kimataifa ya mwaka.
Guardian Angel ambaye huimba nyimbo za injili ameteuliwa kwenye vitengo vinne ambavyo vinajumuisha, msanii bora wa nyimbo za injili, wimbo bora wa injili wa mwaka katika eneo la mashariki ya Afrika, mwandishi bora wa nyimbo za injili mashariki ya Afrika na msanii bora wa kiume wa mwaka.
Mtangazaji wa redio Azeeza Hashim anawania tuzo ya mtangazaji bora wa redio, mfawidhi bora wa hafla za burudani, mtangazi bora wa runinga wa vipindi vya burudani na mwanahabari bora wa mwaka.
Wengine wanaowania tuzo ni Claudia Naisabwa, ambaye pia ni mtangazaji wa runinga na mfawidhi wa hafla za burudani,
Ila Nia, msanii chipukizi na David Fernandez wa Kenya na Rwanda ambaye ni mwelekezi na mwandalizi wa video.
Shughuli ya kupiga kura itaanza rasmi Februari 15 ikamilike Machi 25, 2025.