Wizara ya Afya imeimarisha vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria, kwa kuzindua zoezi la kusambaza vyandarua vya kuzuia mbu katika kaunti 18.
Kulingana na wizara hiyo, itasambaza vyandarua milioni 10.8 ambavyo vimetibiwa na dawa za kuwaangamiza wadudu, katika kaunti ndogo 99, kwa lengo la kukinga familia, kupunguza maambukizi ya malaria na kuchochea juhudi za taifa hili za kutomeza Malaria.
Katibu wa Idaraya Afya na viwango vya utaalam Mary Muthoni, amesema kampeni hiyo inapiga jeki ajenda ya serikali ya kuimarisha utoaji huduma za afya chini ya mpango wa Huduma za Afya kwa Wote (UHC) unaoleta huduma muhimu za afya karibu na jamii.
“Huku taifa linapoimarisha juhudi za kuangamiza Malaria, jamii zinahimizwa kushiriki katika zoezi hili kwa kuchukua vyandarua na kuhakikisha kila mtu analala ndani ya vyandarua kila wakati,” alisema Muthoni.
Kulingana na katibu huyo, vita dhidi ya ugonjwa huo hatari, vinahitaji ushirikiano wa pamoja, na uwekezaji endelevu.
Licha ya hatua zilizopigwa dhidi ya ugonjwa huo hapa nchini, Maralia inasalia kuwa changamoto kuu katika afya ya umma nchini Kenya, ikiathiri mamilioni ya watu kila mwaka.