Watatu wakamatwa kuhusiana na ulaghai wa hoteli na safari

Walimtapeli mlalamikaji kiasi cha milioni 7.98, kupitia madai ya kuweka nafasi za hoteli, mipango ya safari na malipo mengine.

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa upelelezi kutoka makao makuu ya idara ya upelelezi wa jinai hapa Nairobi wamewakamata washukiwa watatu wanaohusishwa na mpango wa ulaghai.

Watatu hao wanaripotiwa kumtapeli mlalamikaji kiasi cha shilingi milioni 7.98, kupitia madai ya kuweka nafasi za hoteli, mipango ya safari na malipo mengine yanayohusiana na huduma hizo.

Washukiwa hao ni Purvis Gaitho Maina, Agnes Seyian Mejooli na Davies Ochami Matasa. Walikamatwa Novemba 13, 2026, katika mji wa Voi, Kaunti ya Taita Taveta, kufuatia uchunguzi kuhusu kisa hicho cha ulaghai.

Kwa mujibu wa uchunguzi, washukiwa hao, wakishirikiana na watu wengine, walitoa taarifa za uongo kwa mlalamikaji na kumshawishi kuwalipa kiasi hicho cha fedha katika tarehe tofauti.

Walijisingizia kuwa wanaotoa huduma halali za kuweka nafasi za hoteli, kupanga safari na huduma nyingine zinazohusiana.

Kukamatwa kwa watatu hao kunafuatia kukamatwa kwa Pascal Omondi Onyango, ambaye alikuwa tayari amekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Milimani kuhusiana na kesi hiyo hiyo.

Washukiwa hao wamezuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kilimani na wanatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Milimani pamoja na mshtakiwa mwenzao kujibu mashtaka ya kupata fedha kwa njia ya udanganyifu, kinyume na Kifungu cha 313 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Share This Article