Miaka miwili baadaye, shinikizo za kuachiliwa kwa Besigye zaendelea

Wanaharakati wameelezea pia wasiwasi kuhusu afya ya Besigye kufuatia hatua yake ya kugoma kula.

Marion Bosire
2 Min Read

Leo Jumatatu, Novemba 16, 2026, inatimia miaka miwili tangu mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Dkt. Kizza Besigye, na msaidizi wake, Hajj Obeid Lutale, kutekwa nyara jijini Nairobi na kuhamishiwa nchini Uganda.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu, wanaharakati wa Kenya na viongozi wa upinzani nchini Uganda wanaadhimisha siku hii kwa kuhuisha wito wa kutaka wawili hao waachiliwe mara moja.

Kwa mujibu wa shirika la Amnesty Kenya, wawili hao walikamatwa katika mji mkuu wa Kenya Novemba 16, 2024, katika operesheni ambayo mamlaka za Kenya zimekanusha kuhusika nayo.

Awali, Besigye alifikishwa katika mahakama ya kijeshi nchini Uganda lakini kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu wa Januari 31, 2025, uliopiga marufuku kuwafungulia kesi raia katika mahakama za kijeshi, kesi yake ya uhaini ilihamishiwa katika mahakama ya kiraia.

Mchakato wa kisheria umekumbwa na utata mbalimbali, ukiwemo kufukuzwa nchini humo kwa wakili mkuu wa utetezi, Martha Karua wa Kenya na kuwekwa kizuizini kwa mawakili wa ndani.

Mashirika ya haki za binadamu na Chama cha Wanasheria nchini Kenya, LSK yamekemea kuendelea kushikiliwa kwao, yakisema ni ukandamizaji wa kisiasa unaovuka mipaka ya nchi na usio halali.

Yameelezea pia wasiwasi kuhusu afya ya Besigye kufuatia hatua yake ya kugoma kula.

Maafisa wa serikali ya Uganda wanasisitiza kuwa hatua zao ni muhimu kwa ajili ya kudumisha usalama na utulivu wa umma.

Share This Article