Mwanamke anayedaiwa kujipatia ardhi inayomilikiwa na kampuni ya kibinafsi kwa njia ya ulaghai, alifikishwa kwenye mahakama ya Milimani siku ya Jumatatu.
Margaret Wairimu Magugu, alishtakiwa kwa makosa kadhaa ikiwa ni pamoja na kusajili kupitia udanganyifu, kughushi na kuwasilisha stakabadhi bandia ya ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Wibeso Investment.
Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Wairimu alipata hatimiliki ya ardhi hiyo mwaka 2021 kupitia ulaghai na kisha kubadilisha umilki wake hadi kwa kampuni ya Marg Ridge Estate Limited, ambayo anaimiliki.
Maafisa wa DCI, walianzisha uchunguzi baada ya malalamishi kutoka kampuni ya Wibeso Investment Limited, iliyoshikilia kuwa ilimiliki ardhihiyo tangu Oktoba 26,1995 na haijawai kuiuza.
Uchunguzi hata hivyo ulibainisha kuwa, mshukiwa huyo aliwasilisha stakabadhi bandia kuashiria alilipa shilingi 824,733 ili kubadilisha umiliki wa ardhi hiyo.
Kesi hiyo itatajwa Julai 30, 2025.