Watu 11 wamepata majeraha na kupelekwa hospitalini, baada ya ukuta kuporomoka katika eneo la Riverside Drive, kaunti ya Nairobi.
Shirika la Msalaba Mwekundu limethibitisha kuwa waathiriwa hao 11, wanapokea matibabu baada ya kuokolewa.
Kulingana na shirika hilo, ukuta huo unadaiwa uliporomoka kwenye eneo la ujenzi, karibu makazi ya Grand Residence.
“Ukuta umeporomoka na maafisa wetu wako kwenye eneo la mkasa kwa usaidizi wa ambulensi mbili za E-Plus,” lilisema shirika hilo kwenye taarifa.
Tukio hilo limejiri siku moja baada ya wafanyakazi sita kufariki baada ya jengo kuporomoka Syokimau, kaunti ya Nairobi.
Mwezi uliopita watu wanane walifariki na wanne kuokolewa wakiwa hai, baada ya jengo kuporomoka Eastleigh, kaunti ya Nairobi.