UAE yaondoa marufuku ya utoaji viza kwa raia wa Uganda

Marufuku hiyo ilikuwa imeanza kutekelezwa Juni 6, 2026, kama hatua ya tahadhari ya kulinda afya ya umma kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda.

Marion Bosire
2 Min Read
Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda

Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE umeondoa rasmi marufuku ya utoaji wa viza mpya za kuingia nchini humo kwa raia wa Uganda, na hivyo kumaliza zuio lililodumu miezi mitano.

Tangazo hilo lilitolewa jana Jumatano, Novemba 11, 2026, na Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Dharura, Migogoro na Maafa ya UAE, NCEMA.

Marufuku hiyo ilikuwa imeanza kutekelezwa Juni 6, 2026, kama hatua ya tahadhari ya kulinda afya ya umma kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda.

Chini ya mwongozo mpya, raia wa Uganda sasa wanaruhusiwa tena kuomba na kupatiwa viza mpya za UAE. Hata hivyo, mamlaka zimeendeleza masharti makali ya uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini humo.

Ili kuruhusiwa kuingia UAE, waombaji wanapaswa kuthibitisha kuwa wamekaa nje ya Uganda kwa angalau siku 21 kabla ya kuwasili katika taifa hilo.

Hata hivyo, misamaha maalumu imeendelea kutolewa kwa wanafunzi waliosajiliwa na familia zao, wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na maalumu, wafanyakazi wa ubalozi wa Uganda, pamoja na watu wanaohitaji matibabu ya dharura au msaada wa kibinadamu baada ya kupata idhini rasmi.

Wakati vikwazo kwa Uganda vikipunguzwa, NCEMA imethibitisha kuwa hatua za tahadhari kuhusu safari na utoaji wa viza bado zinaendelea kutekelezwa kwa mataifa mengine yaliyoathiriwa na milipuko ya magonjwa katika eneo hilo, yakiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan Kusini.

Share This Article