Vinka akanusha madai ya ushindani katika Swangz Avenue

Alisema hachukulii wasanii wenzake wa Swangz Avenue kama wapinzani

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda msajiliwa wa kampuni ya Swangz Avenue, Vinka, amekanusha madai ya muda mrefu kwamba kuna ushindani kati ya wasanii waliosajiliwa na kampuni hiyo.

Vinka ambaye jina lake halisi ni Veronica Lugya Nakiyingi anasisitiza kuwa ushirikiano, sio ushindani na ndio unaochangia mafanikio yao.

Akizungumza katika mahojiano nchini humo, Vinka alisema yeye huwa hachukulii wasanii wenzake wa Swangz Avenue kama wapinzani wake na kwamba ushindani wa kweli upo nje ya kampuni, sio ndani.

“Hii ni lebo ya muziki. Sioni kama kuna ushindani kati yangu na wasanii wenzangu wa lebo hii. Ushindani wetu uko na ulimwengu mzima wa muziki. Hapa tunasaidiana,” alielezea mrembo huyo.

Alifichua kwamba Azawi alimwandikia wimbo Love Panic, na ana nyimbo nne za ushirikiano na Winnie Nwagi.

“Hakupaswi kuwa na ushindani usio na afya. Sisi wote tunasonga mbele kama kundi kwa sababu ni lazima tushinde pamoja kama timu,” alisema.

Vinka alieleza kuwa ushirikiano wa kimuziki na uandishi wa nyimbo ndani ya Swangz Avenue ni thibitisho kwamba wasanii wake wamejikita katika kuinuana badala ya kushindana wenyewe.

Kwa mujibu wa Vinka, umoja uliopo miongoni mwa wasanii wa Swangz Avenue umekuwa nguzo muhimu katika mafanikio na ukuaji endelevu wa lebo hiyo.

Anaamini kuwa kwa kufanya kazi pamoja na kusaidiana katika kukuza taaluma zao, wasanii hao wana nafasi kubwa zaidi ya kushindana na tasnia pana ya muziki kuliko kushindana wao kwa wao.

Share This Article