Timu ya mpira wa wavu ya GSU ilianza kampeni yake ya Kombe la Kenya 2026 katika hatua ya mwondoano kwa kishindo jana.
Hii ni baada ya kuichapa timu mpya ya ligi, Bunge VC, kwa seti 3–0 katika mchezo wa hatua ya 16 bora uwanjani Nyayo.
Baada ya kuaga Ligi Kuu ya Shirikisho la Mpira wa Wavu Kenya,KVF katika hatua ya robo fainali, wawakilishi wa hao wa huduma ya taifa ya polisi walirejea kwa kiwango cha hali ya juu.
Walitawala mchezo kuanzia mwanzo hadi mwisho kwa ushindi wa seti za 25–15, 25–18 na 25–18.
GSU ilinufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa wachezaji wazoefu wa kulipwa, akiwemo Nicholas Matui na Simion Kipkorir ambao walionyesha kiwango kilichozidi wapinzani wao kutoka Bunge.
Mpangaji chipukizi Emmanuel Some alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi kutokana na mchango wake mkubwa katika ushindi huo.
Ushindi huu wa kishindo umeihakikishia GSU nafasi ya kutinga robo fainali ya Kombe la Kenya 2026.
Mashindano yanaendelea leo kwa ratiba ngumu na ya kusisimua, yakihusisha timu nyingine zenye nguvu za huduma ya taifa ya polisi.
Mashabiki wa mpira wa wavu watashuhudia timu za DCI Queens, AP Kenya na KAPU zikicheza mechi zinazotarajiwa kuwa na ushindani mkali.
Wananchi wote wamealikwa uwanjani Nyayo leo kushuhudia burudani ya mpira wa wavu wa kiwango cha juu na kuunga mkono timu wanazozipenda.