Wakazi wa Kigali wanatarajiwa kushuhudia usiku wa kipekee wa burudani ya muziki wa Amapiano na Hip-Hop, burudani itakayoongozwa na nyota wa Afrika Kusini, 031 Choppa.
Choppa ndiye mtumbuizaji mkuu wa tamasha ya maadhimisho ya mwaka mmoja ya The Capital City Rave itakayofanyika Ijumaa, Julai 19, 2026, katika Ukumbi wa Azzurri Club & Lounge.
031 Choppa, ambaye jina lake halisi ni Minenhle Lesley Mnguni mzaliwa wa KwaMashu, Durban, alianza kujulikana kama mtayarishaji wa muziki kabla ya kujijengea jina kama msanii wa kurekodi.
Alipata umaarufu mwaka 2021 baada ya kutayarisha wimbo Super Soft wa AKA na Costa Titch, na tangu wakati huo amefanya kazi na baadhi ya wanamuziki wakubwa wa Afrika Kusini akiwemo Riky Rick, DJ Maphorisa na Sjava. Baadhi ya nyimbo zake maarufu ni Malume, Fast Fast na Hamba No Choppa.
Tamasha hiyo pia itampokea mwimbaji na mtunzi wa nyimbo kutoka Rwanda, Jeroismusic, anayefahamika kupitia nyimbo kama The One, Bambu na Antidote.
Burudani itaongezwa na maonesho ya DJ GRVNDLVNG, DJ Higa, Prince Okuta na DJ YNF, huku DJ Crymez akiwa msimamizi wa shughuli hiyo.
Tamasha hiyo imeandaliwa na The Basement Groove East Africa kwa kushirikiana na Riot Rave, ikiadhimisha mwaka mmoja tangu kuzinduliwa kwa hafla ya burudani ya Capital City Rave mjini Kigali.
Mashabiki pia watapata fursa ya kutazama mubashara fainali ya Kombe la Dunia la FIFA kabla ya burudani kuendelea hadi saa 8 usiku.