Aliyekuwa Seneta wa kaunti ya Pokot Magharibi Samuel Poghisio, amekigura chama cha KANU na kujiunga na chama cha Orange Democratic Movement (ODM).
Poghisio ambaye ndiye mbunge wa kwanza wa Kacheliba, alikaribishwa katika chama cha ODM na Naibu Kiongozi wa chama cha ODM Simba Arati, aliyempongeza kwa ujasiri na kujitolea kwake.
“Baba alipenda Pokot Magharibi. Watu wa Pokot nao walimpenda,” alisema Arati alipompokea Poghisio.
Baada ya kukaribishwa katika chama hicho, Seneta huyo wa zamani alielezea azma yake ya kuwania Ugavana wa Pokot Magharibi kwa tiketi ya chama cha ODM, huku akiahidi kukipigia debe chama hicho katika eneo hilo.
Akizungumza katika jumba la Chungwa Jijini Nairobi, Poghisio alisema alichukua hatua hiyo baada ya mashauriano ya kina na maafisa wa chama hicho katika kaunti hiyo pamoja na familia yake.
Poghisio alikuwa ameandamana na ujumbe wa watu 80, wakiwemo Wawakilishi wadi ambao pia walihamia katika chama cha ODM.