Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Nandy, amemuonya mwanablogu anayeendesha ukurasa unaojiita “Charts Data” akimtaka aache kutumia jina lake katika takwimu anazozitaja kuwa sio za kweli.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nandy alieleza kukerwa na taarifa zinazohusishwa na orodha hizo, akidai zinapotosha kuhusu uwezo wake wa kufanya vizuri katika muziki na mapato ya kazi zake.
Mwimbaji huyo alisema amewahi kumwelekeza mwanablogu huyo awasiliane naye moja kwa moja iwapo anahitaji taarifa sahihi, lakini amesikitishwa na kile alichokitaja kuwa ni kuendelea kuchapisha madai yasiyo na msingi.
Nandy alisisitiza kuwa muziki wake ni biashara na kwamba mapato yanayotokana na kazi zake huingia kwake moja kwa moja.
Alimwalika mwanablogu huyo kufanya mazungumzo ya moja kwa moja kupitia Instagram ili aweze kumweleza kuhusu takwimu na majukwaa ya mapato.
Aidha, msanii huyo alidai kuwa hakuna msanii wa kike aliyefikisha idadi ya mitazamo au usikilizaji wa wimbo wake mmoja mwaka huu, akiwataka wanaotilia shaka madai hayo kukagua takwimu za YouTube.
Kauli hiyo imekuja kufuatia chati au orodha iliyosambazwa mtandaoni kuhusu wasanii wa kike wa Bongo Fleva wenye watazamaji wengi YouTube mwezi Oktoba 2026.
Chati hiyo ilimweka Zuchu katika nafasi ya kwanza kwa watazamaji milioni 37, huku Nandy akiorodheshwa wa pili kwa milioni saba.