Washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati wakamatwa sehemu tofauti

Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema imejitolea kusambaratisha walanguzi wa mihadarati kupitia operesheni za kijasusi.

Tom Mathinji
2 Min Read
Washukiwa wanne wa ulanguzi wa mihadarati wakamatwa sehemu tofauti za nchi.

Maafisa wa asasi mbalimbali za usalama, wamewakamata washukiwa wanne wa ulanguzi wa mihadarati katika kaunti za Kisii, Kitui na Kajiado.

Katika eneo la Riosiri, kaunti ya Kisii, baada ya kupokea habari kutoka kwa wananchi, maafisa wa usalama walivamia makazi ya mshukiwa mmoja akiwa na kilo 1.63 za bangi, lita 70 za pombe aina ya chang’aa, sigara aina ya Supermarch, pakiti 9 za sigara aina ya Oris zinazoshukiwa kuwa za bandia.

Mshukiwa huyo Amos Mogere Omari, anazuiliwa korokoroni akisubiri kufikishwa mahakamani.

Wakati huo huo katika Barabara Kuu ya Thika–Garissa katika eneo la Kanyonyoo, kaunti ya  Kitui, maafisa wa usalama walipata bangi kwenye abiria aliyekuwa kwenye basi lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi kuelekea Garissa.

Uchunguzi wa awali ulibainisha kuwa Dominic Mweu Kimanzi, alinunua Mihadarati hiyo katika eneo la Gatitu, Thika, na alikuwa akiipeleka katika soko la Ukasi Mwingi Mashariki.

Mshukiwa huyo anazuiliwa katika Kituo cha polisi cha Kanyonyoo.

Na katika kaunti ya Kajiado, Maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI), walisimamisha gari ayna ya Toyota Sienta kwenye barabara ya Oloitoktok–Emali baada ya kupashwa habari na wananchi na kupata magunia manne ya bangi.

Washukiwa Daniel Momanyi Mongare, Samwuel Kasane na Mercy Naserian walitiwa nguvuni kuhusiana na mihadarati hiyo.

Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema imejitolea kusambaratisha walanguzi wa mihadarati kupitia operesheni za kijasusi.

Share This Article