Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, amesifu uhusiano mwema kati ya Ethiopia na Kenya, huku akitoa wito wa kuimarishwa kwa biashara kwa ustawi wa mataifa hayo mawili.
Akizungumza leo Jumanne wakati wa sherehe za 63 za Mashujaa katika uwanja wa Kipchoge Keino mjini Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu, Abiy alidokeza kuwa ipo haja ya kuongeza shughuli za kitalii na kuhakikisha ushirikiano dhabiti wa kitamaduni kati ya nchini hizo mbili.
” Ushirikiano wetu unaimarika kupitia biashara. Leo kampuni ya mawasiliano ya Safaricom inawaunganisha mamilioni ya raia wa Ethiopia na mfumo wake wa Mpesa unawasaidia raia hao kutuma na kupokea pesa,” alisema Abiy.
“Tumekuwa majirani kutokana na ramani, huku historia ikitufanya kuwa ndugu. Tunapaswa kuimarisha ushirikiano wetu, kufanikisha ustawi wa pamoja,” alisema Waziri huyo Mkuu.
Alifananisha wakulima wa Kenya na wale wa Ethiopia, akisema wanatekeleza jukumu muhimu la kuhakikisha utoshelevu wa chakula na kuimarisha maisha kupitia shughuli za kilimo.
Sherehe za mwaka huu za Mashujaa zimeandaliwa kwa ushirikiano wa kaunti tatu ambazo ni Nandi, Elgeyo Marakwet na Uasin Gishu, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa sherehe hizo kuandaliwa na kaunti tatu kwa pamoja.