ODPP yaorodhesha kesi za ufisadi zilizo mahakamani juma hili

Hata hivyo taasisi hiyo imefafanua kwamba madai yaliyotajwa hayamaanishi wahusika wamepatikana na hatia.

Marion Bosire
2 Min Read
Renson Ingonga - Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Nchini, ODPP imetoa orodha ya kesi za ufisadi ambazo zitashughulikiwa katika mahakama mbali mbali nchini wiki hii, Oktoba 19 hadi 23, 2026.

Kesi hizo zinahusu madai ya matumizi mabaya ya mamlaka, ubadhirifu wa fedha za umma, hongo, ukiukaji wa taratibu za ununuzi na matumizi ya vyeti vya kitaaluma vinavyodaiwa kughushiwa ili kupata ajira katika taasisi za umma.

Miongoni mwa kesi hizo ni inayomhusu Obindah Frederick Nyedhes, inayohusishwa na madai ya matumizi mabaya ya mamlaka na ubadhirifu wa fedha za umma kutoka Hazina ya Taifa. Kesi hiyo imepangwa kutajwa Oktoba 22 ili mahakama itoe maelekezo.

Kesi nyingine inawahusu John Ngure Kabutha na wengine 36, wanaokabiliwa na madai ya kuidhinisha malipo kwa kampuni kadhaa kinyume cha sheria, itatajwa Oktoba 19 kwa ajili ya kubadilisha masharti ya dhamana.

Orodha hiyo pia inajumuisha kesi zinazohusiana na madai ya kutumia vyeti vya kitaaluma vilivyoghushiwa kupata ajira katika kampuni ya maji na usafi ya Nairobi, Bodi ya Nyuklia ya Kenya na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

Kesi nyingine zinahusu madai ya kutoa hongo kwa afisa wa uangalizi wa wahalifu katika Kaunti Ndogo ya Kangema na ununuzi unaodaiwa kukiuka taratibu wa programu ya kuhifadhi kumbukumbu za ukaguzi na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

ODPP imetoa ratiba hiyo ili kuwafahamisha wananchi kuhusu maendeleo ya kesi zinazohusiana na ufisadi mahakamani. Hata hivyo, madai yaliyotajwa hayamaanishi kuwa wahusika wamepatikana na hatia.

Orodha kamili hii hapa;

Share This Article