Thamani ya shilingi ya Uganda yapungua pakubwa

Kiwango cha ubadilishanaji wa sarafu hiyo sasa kimefikia rekodi ya chini ya shilingi 4,143 kwa dola moja ya Marekani.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Thamani ya Shilingi ya Uganda, imeshuka hadi kiwango cha chini zaidi katika muda wa zaidi ya miongo mitatu, baada ya kuvuka kiwango cha shilingi 4,000 kwa dola moja ya Marekani.

Kiwango cha ubadilishanaji wa sarafu hiyo sasa kimefikia rekodi ya chini ya shilingi 4,143 kwa dola moja ya Marekani.

Kushuka huko kwa kasi kunaashiria kupungua kwa thamani ya shilingi kwa asilimia 10 tangu mwisho wa Agosti, na kuifanya kuwa miongoni mwa sarafu zilizopoteza thamani kwa kiwango kikubwa zaidi duniani katika robo hii ya mwaka.

Wachambuzi wa masoko wanahusisha hali hiyo na utoaji mkubwa wa mitaji nchini humo pamoja na ongezeko la mahitaji ya dola za Marekani kutoka kwa kampuni.

Zaidi ya dola milioni 200 za mitaji ya kigeni zimetolewa katika soko la hati fungani la Uganda ndani ya wiki mbili pekee, kutokana na viwango vya juu vya riba vinavyotolewa na hati fungani za Hazina ya Marekani.

Nchini Uganda, wazalishaji na waagizaji wa nishati wanakimbilia kununua dola ili kufadhili bidhaa za akiba kwa ajili ya mwisho wa mwaka, hali inayosababisha uhaba mkubwa wa ukwasi katika soko la ndani.

Kufuatia hali hiyo, Benki Kuu ya Uganda imetoa tahadhari na kupanga mkutano wa dharura wa Kamati ya Sera ya Fedha ili kushughulikia mgogoro huo.

Badala ya kutumia akiba ya fedha za kigeni kutetea thamani ya shilingi, watunga sera tayari wameongeza kwa kiwango kikubwa mahitaji ya akiba ya fedha taslimu kwa benki za biashara kutoka asilimia 11 hadi asilimia 13.5.

Huku bei za nishati duniani zikiendelea kupanda, wananchi wanakabiliwa na shinikizo la kupanda kwa mfumuko wa bei, huku bidhaa zinazoagizwa kutoka nje zikitarajiwa kuwa ghali zaidi.

Share This Article