Mwanamuziki na mbunge wa eneo la Muheza nchini Tanzania Hamis Mwinjuma au ukipenda Mwana Fa, ndiye waziri mpya wa uvuvi katika serikali ya taifa hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, alifanya uteuzi huo jana Novemba 25, 2026, kufuatia mabadiliko ya muundo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo imegawanywa kuwa Wizara mbili zinazojitegemea.
Haya ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 25, 2026 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais katika Ikulu.
Kabla ya uteuzı huo, Mwana FA alikuwa akihudumu kama Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Aidha, Rais Samia amemteua Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwa Waziri wa Mifugo, huku uapisho wa Viongozi hao ukitarajiwa kufanyika katika tarehe itakayopangwa baadaye.
Mwana FA aliingilia siasa mwaka 2020, alipoamua kuwania Ubunge katika Jimbo la Muheza, na Februari 2023, aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Licha ya majukumu yake ya kisiasa na serikalini, Mwana FA ameendelea kutoa nyimbo na albamu, akishirikiana zaidi na msanii mwenzake wa zamani wa kundi la East Coast Team.
Ameshirikiana kimuziki na wasanii mbalimbali wakongwe na chipukizi wanaotamba nchini Tanzania, akiwemo Maua Sama, Alikiba, Harmonize, Lady Jaydee na Vanessa Mdee na kuachia nyimbo kadhaa zilizofanikiwa pakubwa.