Mshukiwa wa pili katika sakata ya ulaghai wa ardhi ya thamani ya shilingi milioni 25, amekamatwa na maafisa wa upelelezi kutoka Kitengo cha Uchunguzi wa Ulaghai wa Ardhi (LFIU) katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI.
Fatah Farah Ahmed alikamatwa katika eneo la makazi la Nyayo, Embakasi, Nairobi, kufuatia uchunguzi kuhusu jaribio la kujipatia umiliki wa kipande cha ardhi kilichopo Eastleigh kwa njia ya udanganyifu.
Kesi hiyo ilianza baada ya mmiliki wa ardhi hiyo kuwasilisha malalamishi akidai kuwa Ahmed na kampuni ya Skyline Works Limited, walipanga njama ya kunyakua mali yake bila yeye kufahamu.
Ardhi inayozozaniwa ina ukubwa wa takriban futi 50 kwa 100 na iko kando ya barabara ya Fourth Street, Eastleigh Section One. Thamani yake inakadiriwa kuwa shilingi milioni 25.
Baada ya kukamilisha uchunguzi, maafisa wa DCI waliwasilisha faili la kesi kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ODPP, kwa mapitio na maelekezo.
ODPP ilielekeza washukiwa watatu kushtakiwa kwa kosa la kutengeneza hati ghushi.
Kukamatwa kwa Ahmed kunafanya idadi ya washukiwa waliokamatwa kuhusiana na kashfa hiyo kuwa wawili. Mshukiwa mwenzake, Abdul Tahalil, alikamatwa awali.
Wakati huo huo, maafisa wa upelelezi wameimarisha msako wa kumtafuta mshukiwa wa tatu, huku Ahmed akiandaliwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.