Rais William Ruto ameelezea hatua kubwa zilizopigwa katika sekta ya kilimo nchini Kenya katika kipindi cha miaka minne iliyopita, ambazo zimefanikisha utoshelevu wa chakula.
Akizungumza Alhamisi kwenye kongamano la Kilimo na Mageuzi ya Utoshelevu wa Chakula katika uwanja wa Jamhuri Nairobi, kiongozi wa taifa alisema hatua za kijasiri zilizochukuliwa na utawala wake, zimesababisha kuongezeka kwa mavuno ya chakula, huku wakulima wakipata mapato yaliyoimarika.
“Tangu mwaka 2022, tumepunguza bei ya zaidi ya magunia milioni 38 ya mbolea, kutoka shilingi 7,500 hadi shilingi 2,000 na kuwaepusha wakulima dhidi ya bei ghali za pembejeo za kilimo,” alisema Rais Ruto.
Kulingana na Rais, hatua hiyo ilisababisha kuimarika kwa mazao ya mahindi, ambapo uzalishaji wake uliongezeka kutoka magunia milioni 34.3 mwaka 2022, hadi magunia milioni 71 mwaka 2025, huku mavuno ya pamba yakiimarika kutoka kilo 177 hadi kilo 378 kwa kila ekari.
“Hii ndiyo baadhi ya mifano ya mabadiliko inayotekelezwa katika sekta ya kilimo kutokana na miaka minne ya mageuzi na uwekezaji endelevu,” aliongeza kiongozi wa taifa.
Kwenye kongamano hilo, Ruto alisema serikali itajenga mabwawa makubwa, ya kadri na yale madogo kote nchini kwa kutumia hazina ya miundombinu ili kupanua unyunyizaji mashamba maji hadi ekari milioni 2.5, kuhakikisha utoshelevu wa chakula.
Mkutano huo uliwaleta pamoja wadau 10,000 kuangazia hatua zilizopigwa na changamoto zilizopo katika kufanyia mageuzi sekta ya kilimo.