Kenya na Uganda zimekariri azma za kuondoa vizingizti vinavyohujumu biashara kwenye mipaka ya mataifa hayo.
Katibu wa Idara ya Biashara nchini Kenya Regina Ombam, alitoa wito wa kutekelezwa kwa mikakati ya kurahisisha biashara kati ya Kenya na Uganda kwa kuondoa msongamano, uchelewashi na vikwazo vingine mipakani.
Akizungumza kwenye mkutano wa pili wa kiufundi wa pamoja, Ombam alielezea kujitolea kwa Kenya kutekeleza maazimio ya mkutano huo wa kiufundi kuhusu kituo kimoja cha mpakani na ushuru unaobagua.
“Makubaliano haya hayatatekelezwa kwa bahati, lazima tuendelee na moyo wa ushirikiano,” alisema Ombam.
Kwa upande wake, Katibu katika Wizara ya Biashara nchini Uganda Lynette Begoza, alisema taifa lake linalenga kuimarisha biashara kati yake na Kenya, akidokeza kuwa biashara kati ya mataifa hayo mawili iliimarika kutoka dola milioni 76 za Marekani hadi dola milioni 592.3 katika nusu ya mwaka wa kifedha 2025/26.
“Uganda hailengi kupunguza biashara, lakini kupanua biashara,” alisema Begoza.
Alitoa wito kwa pande hizo mbili kutekeleza kikamilifu maazimio ya mkutano huo katika muda uliowekwa na taasisi husika.