Murkomen asema ugatuzi wa huduma za paspoti unaendelea

Huduma hizo kwa sasa zinapatikana Mombasa, Kisumu, Eldoret, Kericho, Embu, Bungoma, Kisii, Nakuru na Garissa.

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, amesema serikali inapiga hatua katika kugatua huduma za utoaji wa pasipoti ili kuzifikisha karibu na wananchi.

Murkomen alisema mageuzi hayo yalijadiliwa katika mkutano na maafisa wa Idara ya Huduma za Uhamiaji, ambapo walikagua hatua zinazoendelea za kuboresha utoaji wa huduma.

Alisema ofisi za kikanda za pasipoti zinafanya kazi kwa sasa katika miji kama Mombasa, Kisumu, Eldoret, Kericho, Embu, Bungoma, Kisii, Nakuru na Garissa.

Kwa mujibu wa Murkomen, ofisi nyingine za pasipoti zinapangwa kufunguliwa huko Malindi na Nyeri, huku serikali ikiendelea kupanua upatikanaji wa huduma hiyo.

Pia alisema Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira imeanzisha vituo maalum katika ofisi za Uhamiaji jijini Nairobi ili kusaidia katika mpango wa Kazi Majuu.

Mageuzi mengine yanahusisha usakinishaji unaoendelea wa milango ya kielektroniki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA, mageuzi yanayotarajiwa kuwezesha kuhudumiwa kwa haraka kwa wasafiri wanaotumia uwanja huo.

Murkomen alikuwa ameandamana na Katibu Mkuu wa Uhamiaji na Huduma za Raia, Dkt Belio Kipsang, pamoja na maafisa wengine wakuu wa serikali.

Share This Article