Kaka mdogo wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Jenerali Salim Saleh anaongoza mazungumzo ya faragha ya viongozi wa serikali na upinzani yanayolenga kumwachilia Kizza Besigye.
Mazungumzo hayo, yaliyoanza wiki iliyopita, yamekutanisha viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na wazee mashuhuri, huku juhudi zikiongezeka kutafuta suluhisho la suala la kuendelea kuzuiliwa kwa Besigye anayeugua.
Kwa mujibu wa taarifa, mazungumzo hayo yanahusisha wawakilishi wa chama tawala cha National Resistance Movement, NRM, chama cha People’s Front for Freedom, PFF na kile cha Forum for Democratic Change, FDC.
Saleh, ambaye ni mratibu wa kitaifa wa mpango wa kukuza utajiri wa ‘Operation Wealth Creation’, anaungwa mkono na kamati ya watu mashuhuri, huku upande wa upinzani ukiunda timu yake ya kushirikiana na kundi lake.
Naibu msemaji wa FDC, Walid Mulindwa, alithibitisha kuwepo kwa mazungumzo hayo, akisema viongozi wa shirika la majadiliano la Inter-Party Organisation for Dialogue, IPOD, pia wanahusika.
Mulindwa alisema wajumbe wa IPOD, wakiwemo makatibu wakuu wa vyama vya siasa, wamejadili suala la kuachiliwa kwa Besigye, suala linalotarajiwa kujadiliwa katika mkutano ujao wa kilele wa taasisi hiyo.
Hata hivyo, masharti ya kuachiliwa kwa Besigye na muda wa kukamilika kwa mazungumzo hayo bado havijabainika.