Polisi wachunguza kifo cha mwanafunzi wa Makerere

Mwili wa mwanafunzi huyo ulipatikana ndani ya eneo lililozungushiwa uzio lenye mnara wa mawasiliano ya simu karibu na Maktaba Kuu ya chuo hicho kikuu nchini Uganda.

Marion Bosire
2 Min Read

Wapelelezi utoka idara ya polisi nchini Uganda wanaoshughulikia mauaji wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Makerere kwa jina Kabuye Kelvin Charles.

Mwili wa Kabuye ulipatikana ndani ya eneo lililozungushiwa uzio lenye mnara wa mawasiliano ya simu karibu na Maktaba Kuu ya chuo hicho.

Marehemu alikuwa mwanafunzi wa Shahada ya Usanifu Majengo katika Chuo cha Uhandisi, Ubunifu, Sanaa na Teknolojia, CEDAT.

Katika taarifa ya tarehe 30 Septemba 2026, chuo hicho kikuu kilisema mwili wa Kabuye uligunduliwa mapema Jumatatu Septemba 28, 2026 ndani ya eneo lililozungushiwa uzio linalohifadhi mnara wa MTN, mkabala na Maktaba Kuu.

Idara ya usalama katika taasisi hiyo ya elimu ya juu, iliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Makerere, na polisi wakafika eneo la tukio.

“Maafisa wa polisi waliitikia mara moja na kukabidhi uchunguzi kwa Kitengo cha Mauaji cha Wandegeya pamoja na Maafisa wa Uchunguzi wa Eneo la Tukio,” chuo hicho kilisema.

Chanzo cha kifo cha Kabuye bado hakijajulikana.

Makerere ilisema wachunguzi wameomba uchunguzi wa mwili ili kubaini chanzo cha kifo, na kuahidi kuendelea kushirikiana na polisi huku uchunguzi ukiendelea.

Uongozi wa bweni la Nkrumah katika chuo hicho ulithibitisha awali kwamba Kabuye alikuwa mkazi wa Chumba nambari C34 katika jengo hilo maarufu.

Share This Article