Raia wa Uganda wameungana kwa njia ya kipekee kumwokoa msomi, mchora vibonzo na mwanaharakati wa kijamii nchini humo Dkt. Jimmy Spire Ssentongo.
Hii ni baada ya Mahakama Kuu kumuamuru kulipa jumla ya shilingi milioni 30 pesa za Uganda kwa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, KIU, katika muda wa siku 14 la sivyo akabiliwe na kifungo cha miezi mitatu gerezani.
Kampeni ya kuchangisha fedha iliyoanzishwa na mwanaharakati Agather Atuhaire ilikusanya shilingi milioni 24 katika muda wa saa 24, hivyo kubakisha milioni 6 pekee kufikisha kiasi kilichoamriwa na mahakama.
Kesi hiyo ilitokana na machapisho ya Ssentongo kwenye mitandao ya kijamii, ambapo aliibua malalamiko yaliyohusu KIU.
Oktoba 2025, alichapisha malalamiko ya mwanafunzi aliyedai kuwepo kwa matatizo katika kurejeshewa ada, jambo lililowafanya wanafunzi wa sasa na wa zamani kujitokeza na kulalamikia adhabu kubwa za kuchelewa kulipa ada, uidhinishaji wa kozi, upungufu wa wafanyakazi na michango ya NSSF kutowasilishwa.
Baadaye, KIU ilimshtaki Ssentongo kwa kashfa na kuomba fidia kubwa.
Novemba 2025, Mahakama Kuu ilitoa amri ya muda iliyomzuia kuchapisha taarifa zisizo na uthibitisho au maudhui yanayoweza kuharibu sifa ya chuo hicho.
Mnamo Machi 2026, Ssentongo aliandika kuhusu mgogoro mwingine wa ada uliowahusu wana wa marehemu kakake. Alidai kuwa shilingi milioni 15.57 zilizolipwa kama ada hazikuhamishwa ipasavyo baada ya wanafunzi hao kuhamia chuo kingine.
KIU ilimtuhumu kwa kukiuka amri ya mahakama na kuanzisha kesi ya dharau ya mahakama.
Mnamo Juni mwaka huu, mahakama ilimpata na hatia ya kudharau mahakama na baadaye ikamuamuru alipe faini ya shilingi milioni 10 na milioni nyingine 20 za fidia.
Uamuzi huo umekosolewa na watetezi wa haki za binadamu na viongozi mashuhuri, akiwemo Winnie Byanyima na Robert Kyagulanyi, ambao wanasema kesi hiyo imeibua wasiwasi kuhusu uhuru wa kujieleza.